Wednesday, 29 April 2015

TANZANIA, DOLAR KUPOLOMOKA HUKU SIO KUSHUKA


Mbatia aitaka Serikali itoe tamko anguko la shilingi


mbatiaPatricia Kimelemeta na Shabani Matutu
WAZIRI kivuli wa Fedha, James Mbatia ameitaka Serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa tamko kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi hali ambayo inahatarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbatia alisema kama Serikali itashindwa kufanya hivyo, atawasilisha taarifa kwenye kikao kijacho cha Bunge mjini Dodoma kinachotarajiwa kuanza Mei 12 ili wabunge wajadili suala hili.
Alisema mzunguko wa fedha za kigeni unaongezeka siku hadi siku, huku shilingi ya Tanzania ikiendelea kushuka hali ambayo inahatarisha uchumi.
“Naiomba Serikali itoe tamko juu ya anguko la thamani ya shilingi, hali hii inahatarisha uchumi wa taifa na wananchi wataishi katika mazingira magumu,” alisema.
Mbatia alisema hali hiyo inaonyesha wazi kuwa gharama za maisha zinaweza kupanda wakati wowote kuanzia sasa.
Alisema Serikali inaendelea kufanya manunuzi kwa kutumia fedha za kigeni, jambo ambalo limechangia kushuka thamani ya shilingi.
Mbatia alisema samani ambazo zinatengenezwa nchini, baadhi ya watendaji wananunua kutoka nje ya nchi, hali ambayo inaonyesha wazi Serikali haithamini sarafu yake.
“Licha ya kuiambia mara kwa mara Serikali kuacha kutumia fedha za kigeni katika manunuzi, bado kuna baadhi ya watendaji wanatumia fedha hizo kwenye malipo na manunuzi,” alisema.
Alisema hali hiyo inachangia kushuka kwa thamani ya shilingi na kuzipandisha hadhi fedha za kigeni katika mzunguko wa kila siku.
Mbatia alisema licha ya kufanya manunuzi kwa fedha za kigeni, pia shilingi ya Tanzania imepoteza sifa kutokana na kuongezeka vitendo vya ufisadi, jambo ambalo limesababisha baadhi ya nchi wahisani kukataa kutoa misaada.
Alisema sakata la ufisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow limechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo, kwani baada ya wahisani kugoma kutoa fedha, taifa limejikuta njia panda.

0 comments:

Post a Comment