Sunday, 18 January 2015

MATOKEO KIDATO CHA PILI 2014


 
                       KUANGALIA MATOKEO BOFYA HAPA CHINI
 
 
                                  ANGALIA MATOKEO HAPA
 
 

WANAFUNZI 29,770 waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2014, wamepata alama ambazo haziwawezeshi kuendelea na kidato cha tatu hivyo watalazimika kurudia kidato hicho cha pili.

Sambamba na hilo, matokeo yaliyotolewa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde zimeonesha kuwa ufaulu wa masomo ya Hisabati, Sayansi, Kilimo na Biashara upo chini ya asilimia 50.

Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari jana, Dk Msonde alisema ufaulu kiujumla umeongezeka kwa asilimia 3.32.

Alisema jumla ya watahiniwa 375,434 ambao ni asilimia 92.66 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo mwaka jana wamepata alama zinazowawezesha kuendelea na masomo ya sekondari kidato cha tatu.

Kati ya hao wasichana ni 195,328 (asilimia 92.63) na wavulana ni 180,106 (asilimia 92.69): Mwaka 2013, watahiniwa walioweza kupata alama za kuendelea na kidato cha tatu walikuwa 422,446 ambayo ni asilimia 89.34 ya watahiniwa 472,833 waliofanya mtihani. Waliorudia kidato cha pili walikuwa ni asilimia 10 (zaidi ya wanafunzi 47,000).

Akizungumzia ufaulu wa kimadaraja, Dk Msonde alisema idadi ya wanafunzi waliopata madaraja mazuri ya ufaulu (Distinction, Merit na Credit) ni 180,965 ambao ni asilimia 44.66 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo.

Ufaulu wa juu ni wanafunzi 35,656 (asilimia 8.80), ufaulu wa kati ni 57,945 (asilimia 14.30), ufaulu wa kawaida ni 87,364 (asilimia 21.56), ufaulu wa chini ni 194,469 (asilimia 47.99).

Kuhusu ufaulu wa kimasomo, Msonde alisema watahiniwa wamefaulu zaidi katika masomo ya Uraia, Historia, Kiswahili, Kiingereza ambapo ufaulu huo uko kati ya asilimia 84, huku masomo ya Jiografia, Baiolojia, Utunzaji Hesabu ufaulu wa masomo upo kati ya asilimia 50 hadi 70 wakati ufaulu wa masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia, Sayansi ya Kilimo na Biashara ufaulu wa masomo uko chini asilimia 50.

Alipoulizwa kama Necta imebaini sababu za wanafunzi kufanya vibaya katika masomo hayo, alisema majibu ya maswali yaliyojibiwa na wanafunzi yanaonesha kuwa wanafunzi hawana uelewa wa kina wa masomo, wanashindwa kuelewa maswali na stadi za masomo hayo sio nzuri.

“Tumekuwa na majibu ya kuhisi kuwa huenda hali hii inachangiwa na upungufu wa walimu, lakini ukiangalia majibu ya wanafunzi inaonesha kabisa stadi za wanafunzi sio nzuri, hivyo ni vyema watafiti wakakaa na kuangalia kwa kina ili kubainia sababu za ziada,” alisema.

Aidha, Dk Msonde alisema ufaulu wa juu zaidi ni wa somo la historia ambao ni asilimia 90.71 ya watahiniwa waliofanya somo hilo na ufaulu wa chini ni wa somo la hisabati ambalo ni asilimia 18.15 ya watahiniwa waliofanya somo hilo.

Dk Msonde alisema baadhi ya watahiniwa wameonesha umahiri wa juu katika baadhi ya masomo kwa kupata alama 100, ambapo watahiniwa 41 ni kwenye somo la Kiingereza, tisa katika somo la Hisabati, huku masomo ya Biolojia, Uraia na Utunzaji Hesabu kuna mwanafunzi mmoja mmoja aliyepata alama 100.

Alama 10 za kila somo katika Mtihani wa Kidato ya Pili, huchangia katika Tathimini Tamati ya Mtihani wa Kidato cha Nne kama sehemu ya alama endelevu ya mwanafunzi.

Mtihani wa Kidato cha Pili wa 2014 ni wa kwanza kusimamiwa na Necta. Awali ulikuwa ukiendeshwa na Idara ya Ukaguzi wa Elimu kuanzia mwaka 1999 uliporejeshwa baada ya kusitishwa mwaka 1994.

0 comments:

Post a Comment